Canalblog
Editer l'article Suivre ce blog Administration + Créer mon blog
Publicité
zone verte
zone verte
Archives
Derniers commentaires
19 février 2008

« Peopleisation » : ugonjwa mpya wa waandishi wa habari

« Peopleisation » ni neno jipya nchini Ufaransa. Limebuniwa kutoka neno la Kiingereza « people » miongoni mwa miaka 2000, na maana yake ni kujulisha maisha yasiyo rasmi ya watu wasio nyota. Inaonekana kwamba ni ugonjwa mpya wa waandishi wa habari.

Dhana ya kisasa. “Peopleisation” ni dhana ya kisasa. Kwa hivyo Wafaransa hutumia neno jipya, tangu mwaka 2000 hivi. Na leo hatuwezi kuongea kuhusu hali hiyo bila ya kuzungumzia mtu mmoja, ambaye yumo katika mawazo ya Wafaransa tangu mwezi wa Mei mwaka 2007, yaani Nicolas Sarkozy. Yule mtu ana akili nyingi, hasa akili ya kucheza na waandishi wa habari. Na waandishi hao hurukwa na akili. Ndani ya magazeti, tunaweza kusoma makala kuhusu maisha ya rais, likizo za rais, wapenzi wa rais... kama tunavyoweza kusoma kwa mfano kuhusu nyota wa muziki. Au wachezaji nyota, kama vile Laure Manaudou, msichana bingwa kwa mara nyingi wa mbio za kuogelea. Monique Dagnaud, mchunguzi katika CNRS, kituo cha kitaifa cha utafiti wa kisayansi, alijaribu kueleza hali ya Laure Manaudou. Aliandika kwamba magazeti ya kifaransa hayamheshimu msichana huyo. Badala ya kumhoji kuhusu kazi yake, waandishi wengi wa habari humhoji kuhusu wapenzi wake. Wanataka kuonyesha maisha yake yasiyo rasmi, kwa sababu yanawavutia Wafaransa wanaokimbilia madukani kununua gazeti litakalowaarifu habari nyingi kuhusu maisha ya bingwa huyo wa mabwawa ya kuogelea. 

Namna ya kuchuma hela. Lililowavutia wasomaji, litawavutia waandishi vile vile. Ni mambo ya uchumi. Magazeti yanayohusu « peopleisation » yanauza ndoto laini, ndoto kwamba « nyota iko karibu na mimi, kwamba nyota ni kama mimi ». Hata rais ana shida za kimapenzi. Hata bingwa Laure Manaudou anazo. Kwa hivyo msomaji anaweza kudhani : « Nina maisha yanayofanana na maisha ya Laure ». Nani Ufaransa ambaye hakuona picha ya mama Segolène Royal, mgombea wa urais mshindani wa Sarkozy, akiwa ufukoni mwaka wa 2006 akivaa sidiria na chupi ? Kwa kuchapisha tu picha hiyo, gazeti Closer liliuza magazeti 650 000, badala ya 400 000 ya kawaida. Hata hivyo, nani alijua mpango wa kisiasa wa Segolène Royal ? Siasa nchini Ufaransa sasa inafanana na siasa ya kimarekani. Na hali hiyo imeongezeka zaidi tangu rais mpya Nicolas Sarkozy alipofika madarakani. Inaonekana kwamba anapenda picha yake ichapishwe kwenye magazeti mbalimbali. Lakini, vile vile, inaonekana waandishi wamechoka kuchezacheza kama paka na panya.

Rais alishtaki gazeti la Nouvel Observateur. Mwandishi wake mmoja aliandika kwamba kabla ya ndoa yake mpya, Nicolas Sarkozy alimtumia mkewe wa zamani ujumbe mfupi kwa simu ya mkono ufuatao: «Ukinirudia, sitafunga ndoa». Ujumbe huo eti alimwandikia bibi yake wa kwanza, Cecilia Sarkozy, kabla ya kufunga pingu za maisha na mke wake wa leo, Carla Bruni. Rais alikasirika, na mwandishi wa Nouvel Observateur anaendelea kusema kwamba habari yake ni ya kikweli. Na hapo paka hataki kucheza tena.

Mambo ya hatari. Paka ni mnyama wa hatari. Yeye peke yake anapanga kanuni za mchezo huo. Asipotaka kucheza, yeye peke yake huamua. Tutatoa mfano wa wakati wa mkutano wa kwanza na wanahabari wa tarehe 8 Januari 2008. Suali la pili lilikuwa kuhusu tarehe ya ndoa ya Nicolas Sarkozy na mrembo Carla Bruni. Lilitolewa kabla ya masuali juu ya mambo ya kigeni, mambo ya kiuchumi... Na rais alitangaza : «Mtaarifiwa nitakapokuwa nimefunga ndoa. Siyo gazeti la Journal du Dimanche ambalo litapanga tarehe gani [nitaoa]». Mara hiyo, rais aliwashinda wanahabari.

Uchaguzi wa mabadiliko. Uchaguzi  wa viongozi wa Manispaa Ufaransa ulibadilisha hali kidogo. Kabla ya Jumapili 9 mwezi Machi, uchunguzi wa maoni ulionyesha kwamba rais Sarkozy hakupendwa sana tena. Wafaransa hawakuvumilia kumwona pahali popote na hasa katika mambo yasiyohusu siasa ya taifa! Haidhuru, wapiga kura walichagua kwa jumla chama cha kushoto (wasoshalisti) nchini kote. Tangu siku hiyo, inaonekana Nicolas Sarkozy amepata somo. Sasa anajificha kidogo. Hata kama mke wake hupamba karatasi za kwanza za magazeti maarufu siku hizi.

Mchezo huo ungewachekesha watu wa nchi zote, lakini kwa kweli ni wa hatari sana. «Peopleisation» ni kiini macho. Inazuia wasomaji wasifikirie kuhusu mambo mengine. Kwa mfano matatizo ya kila siku, shida ya kununua gari, nyumba, hata kupata mkate wa kula. Inaficha matatizo ya ajira , ya mambo ya uhamiaji... Wakati rais akitutumia kadi za posta kutoka likizo yake Misri, tunasahau shida nyingine. Lakini likizo ya rais siyo likizo ya Wafaransa wa kawaida. Mke wa rais siyo mke wake jirani yangu. Na la muhimu zaidi ni mawazo ya rais siyo mawazo ya Wafaransa. Hali vichwa vyetu vinatingwa, mikono yake inabaki huru.

Publicité
Commentaires
L
Ahsante Mwalimu!
K
Hongera Laulotte kutupelekea makala hii nzuri juu ya "peopleisation" tena kwa Kiswahili.
Publicité
Publicité